Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Tanga, 04 Agosti 2025 - Usiku wa leo Mkoani Tanga - Korogwe, umeandikwa katika historia kama mwenyeji wa Hafla Kubwa ya Kitaifa ya kuadhimisha Kuzaliwa kwa Mtume wa Daraja na Mkarimu, Muhammad Al-Mustafa (s.a.w.w).
Hafla hii adhimu imehudhuriwa na mamia ya waumini na wapenzi wa Mtume (s.a.w.w) kutoka kila kona ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Miongoni mwa waliohudhuria ni Masheikh, Walimu wa dini, Mabalozi, viongozi wa taasisi mbalimbali, pamoja na watu maarufu waliokusanyika kwa nyuso zenye bashasha, wakifurahia kwa pamoja neema ya kuzaliwa kwa Mtume wa Rehma.
Aidha, miongoni mwa wageni waliohudhuria hafla hiyo alikuwa ni Rais wa Jamiat al-Mustafa (s) Tawi la Dar es Salaam - Tanzania, Hujjatul Islam Sheikh Dkt. Ali Taqavi, aliyeongozana na Sayyid Arif Naqvi, kufuatia mwaliko rasmi kutoka kwa Mheshimiwa Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubair bin Ali.
Sherehe hiyo ya Mazazi ya Mtume wa Ummah (saww), imeonesha mshikamano, mapenzi ya dhati, na hamasa kubwa ya waislamu katika kuenzi maisha na mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w). Idadi kubwa ya washiriki katika hafla hii imekuwa ishara tosha ya mafanikio makubwa ya tukio hilo takatifu, na ushahidi wa mapenzi ya kweli kwa Mtume wa Mwisho.
Katika hotuba na mawaidha yaliyotolewa, wito umetolewa kwa waislamu kuiga maisha ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), hasa katika nyanja za huruma, haki, uadilifu na mshikamano wa kijamii.
Hafla hiyo imehitimishwa kwa dua, kaswida, na salawati, huku wageni wakiondoka wakiwa na furaha, utulivu wa nafsi, na kumbukumbu nzuri ya maadhimisho haya matukufu.
Your Comment